Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya siku tano ya kunyesha mvua kubwa inayoweza kusababisha athari ikiwemo mafuriko.
Taarifa iliyotolewa na TMA imesema kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha Machi 29 hadi Aprili 2, 2019 na kwamba zinaweza kuleta athari kwenye makazi ya watu.
Mvua hiyo inatarajiwa kunyesha katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Zanzibar.
Aidha, taarifa imesema kuwa mvua hizo zinaweza kuleta shida katika usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Imeeleza kuwa Aprili Mosi hadi Aprili 2, 2019 mvua hizo zitanyesha katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Zanzibar.
Hata hivyo, TMA imeishauri Menejimenti ya Maafa na watoa huduma za dharura pamoja na wadau wengine kuchukua hatua za kuweka mipango stahiki kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.