Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa onyo kwa baadhi ya Watendaji Kata na askari nchini ambao wamekuwa wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu waliowapa ujauzito wanafunzi na amesema watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ameyasema hayo jana, wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilula Sokoni, wilayani Kilolo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

“Wanafunzi bado wanaendelea kupewa ujauzito na kukatishwa masomo yao huku watu waliohusika na vitendo hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu baadhi ya watendaji na askari wamezikalia kesi zao na kushindwa kuwafikisha polisi.”

“Watoto wa kike lazima walindwe ili wamalize masomo yao waje kulitumikia Taifa lao, Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi.” Amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na adhabu iliyowekwa na Serikali ni kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayemuoa, kumpa ujauzito na hata ukikutwa naye nyumbani kwako au katika nyumba ya wageni.

Kabla ya kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa mradi wa maji Ilula na kuweka jiwe la msingi. Pia alikagua shughuli za ukarabati wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi  Ilula.

 

 

Tanazania yavunja rekodi ya Uganda 'JAMAFEST'
Video: Dkt. Mpango awapa neno PPRA kwa kuokoa mabilioni, 'Nitamwambia Rais Magufuli'