Serikali imesema kuwa itaongeza ufuatiliaji na kuvichukulia hatua za kisheria vyombo vya habari ambavyo havitazingatia sheria na maadili ikiwa ni pamoja na watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2020/2021, bungeni jijini Dodoma, jana Aprili 22, 2020.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji wa sheria katika maudhui yanayowekwa mitandaoni hali ianyosababisha changamoto kubwa.
“Uwepo wa matumizi ya mitandao ya kijamii usiozingatia sheria zilizopo na matakwa ya kimaadili bado ni changamoto kubwa,” alisema Dkt. Mwakyembe.
“Wizara imeendelea kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu na miongozo ya uchapishaji na matumizi ya taarifa hususan kwenye mitandao ya kijamii,” aliongeza.
Waziri Mwakyembe alisema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itaongeza ufuatiliaji wa maudhui yanayowekwa kwenye mitandao na kwenye vyombo vingine vya habari nchini na kuchukua hatua stahiki.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2018, Serikali imefanya maboresho na kufanikisha mchakato wa utungaji sheria zinazosimamia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya Mwaka 2015, na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016.
Aidha, Waziri Mwakyembe alitoa wito kwa wadau kuboresha maudhui ya ndani ya nchi na kuhamasisha uandaaji wa vipindi zaidi vinavyohusu uchaguzi ujao.
Waziri Mwakyembe aliwasilisha Makadirio ya Bajeti na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/2021 ikiwa ni kiasi cha Sh. 40.14 bilioni.
Pamoja na mambo mengine, bajeti hiyo pia itasaidia kuboresha uandaaji wa maudhui na uendeshaji wa vyombo vya habari vya umma kwa mfumo wa kisasa. Vyombo hivyo ni pamoja na Shirika la Habari Tanzania (TBC) na Tanzania Standard Newspapers (TSN) ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Habari Leo na Spoti Leo.