Kijana Enock Asenga (17) amefariki dunia, kwa kuungua moto akiwa amelala ndani ya duka alilokuwa akiuza lililopo eneo la Sanawari jijini Arusha.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shana amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema moto huo ulizuka ghafla leo Mei 16, majira ya saa 8:00 usiku na kusababisha kifo cha muuza duka huyo.
Amesema, baada ya moto huo kuzuka polisi na kikosi cha zima moto walifika eneo hilo na kushirikiana na wananchi kuzima moto huo kabla haujasambaa kwenye vyumba vingine.
Bidhaa zote zilizokuwa ndani ya duka hilo ikiwemo mitungi ya gesi zimeteketea kwa moto.
Kamanda Shana ameeleza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa ya Mt Meru.