Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaapisha Mawaziri 13 wa Baraza la Mawaziri la serikali ya awamu ya nane na kuwapa magizo ya kuanza nayo katika Wizara zao.
Hafla ya uapisho wa mawaziri hao imefanyika leo Novemba 21, 2020 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini.
Dkt. Mwinyi amewataka mawaziri hao kuhakikkisha kuwa kila mmoja anaijua Wizara yake na Taasisi zilizo chini ya Wizara husika haraka iwezekanavyo kwa kuzitembelea na kutatua changamoto zilizopo na kuwaagiza kufanya kazi kwa weledi na kupambana na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za Umma kwa manufaa ya Taifa.
Aidha, Dkt. Mwinyi amewataka Mawaziri hao kutengeneza Mpango kazi na Bajeti kwa kutumia ilani, hotuba ya Rais, ahadi zake wakati wa kampeni, maoni ya Wadau wa wizara pamoja na kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020/2050.
“Mara baada ya hafla hii ya kula kwenu kiapo, mtapewa kitabu kutoka ofisi yangu chenye ahadi yangu wakati wa kampeni ili mtumie wakati wa kutengeneza mpango kazi na bajeti,” amesema Dkt. Mwinyi.
Mawaziri hao walioapishwa leo Novemba 21 waliteuliwa Novemba 19, 2020 ambapo nafasi mbili za Wizara ya Afya na Wizara ya Biashara ziliachwa wazi kwa ajili ya Chama cha ACT- Wazalendo na bado hazijajazwa mpaka sasa.