Kocha mkuu wa Ruvu Shooting Charles Boniface Mkwasa, amesema ni mapema mno kwa timu yake kuingizwa kwenye mchakato wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.
Ruvu Shooting imekua na mwendelezo mzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu, kwa kufikisha alama 19 ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya nne nyuma ya mabingwa watetezi Simba SC wenye alama 23, wakitanguliwa na Young Africans wenye alama 24, huku Azam FC wakiongoza msimamo kwa kufikisha alama 25.
Ruvu Shooting imefika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kuibanjua Mbeya City juzi Jumamosi (Novemba 21), mabao matatu kwa sifuri Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam.
Kocha Mkwasa amesema kulingana na mwenendo huo, anaamini wadau wa soka nchini wameanza kuipa nafasi Ruvu Shooting kwenye mbio za ubingwa msimu huu, lakini kwake hafikirii hilo.
Mkwasa amesema amefanya maandalizi ya kupambana na ushindani na vile vile kutafuta matokeo mazuri katika kila mchezo ili kumaliza kwenye nafasi nzuri.
“Kwa sasa tunafikiria kutafuta matokeo katika mechi ili kumaliza ligi bila ya presha, kwa msimu huu hatuna wazo la ubingwa sababu ya maandalizi tuliyoyafanya mwanzoni mwa msimu huu, kwa ajili ya kutafuta matokeo ambayo tutaendelea kubaki katika ligi pamoja na kuandaa vijana,” amesema Mkwasa.
Ameongeza kuwa, uamuzi wa kuwaamini wachezaji vijana umemsaidia kufanya vyema na ataendelea kuwapa nafasi kwa sababu timu hiyo inasimamiwa na taasisi ambayo haina uwezo wa kusajili nyota wa kulipwa ambao wanahitaji kulipwa gharama kubwa.
“Kuwaamini vijana katika timu yangu na kunipa matokeo mazuri ni jambo la kujivunia, hii sio kwa ajili ya Ruvu pekee pia watakuja kutusaidia hapo baadaye katika timu zetu za Taifa watakapoonekana na kuaminika,” amesema Mkwasa.