Kiongozi wa zamani wa Baraza la jeshi nchini Mali, Kanali Assimi Goïta, amejitangaza kuwa Rais wa mpito wa nchi hiyo baada ya kuwavua madaraka Rais wa mpito na Waziri Mkuu.
Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane sasa wameachiwa huru na jeshi.
Walipelekwa katika kambi ya kijeshi usiku wa Jumatatu katika hatua ambayo iliifanya Mali kukabiliwa na mapinduzi ya pili ya kijeshi ndani ya miezi tisa.
Hatua hiyo ilichochewa na mageuzi katika baraza la mawaziri ambapo maafisa wawili wa jeshi waliohusika na mapinduzi ya awali walipoteza kazi zao.
Kanali Goïta alilalamika kwamba Rais aliyeondolewa madarakani hakushauriana naye kuhusu baraza jipya la Mawaziri .
Hali ya taharuki imetanda nchini Mali hivi leo lakini kuna utulivu.