Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, umeazimia kuzima ndoto za klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, inayotajwa kujipanga kumsajili Beki kutoka nchini Kenya Joash onyango Achieng, ambaye amekua muhimuli mkubwa kwenye safu ya ulinzi ya Msimbazi.
Onyango amekua chaguo la kwanza kwenye orodha ya usajili wa klabu ya Orlando Pirates, kufuatia kiwango alichokionesha wakati wa ushiriki wa Simba SC kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, msimu huu 2020/21.
Uongozi wa Simba SC umefikia maazimio ya kumsainisha mkataba mpya beki huyo aliejiunga na klabu hiyo akitokea Gor Mahia ya nchini kwao Kenya mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuona hakuna umuhimu wa kumuuza katika kipindi hiki ambacho ameshaiwatumikia wanamsimbazi kwa mwaka mmoja, huku akiwa na mkataba wa miaka miwili.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC, zinaeleza tayari Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez amempa taarifa Onyango kupitia Barua Pepe (Email), pamoja na wakala wake aliopo Kenya juu ya nia yao hiyo.
“Tayari tumewataarifu Onyango na wakala wake kupitia barua pepe kuwa tunahitaji kumuongeza mkataba mpya wa miaka miwili ambao utaanza mara baada ya huu wa sasa kumalizika,”
“Mkataba wa awali ulikuwa wa miaka miwili ambao utamalizika mwisho wa msimu ujao lakini kutokana na kiwango bora alichoonyesha Onyango tumeamua kumuongeza mwingine wa miaka miwili ambao utamalizika 2024,” alisema amtoa taarifa na kuongeza.
“Tumefanya hivyo kutokana na timu kuhitaji mchango wake lakini kama kuna ambao watakuwa wanataka huduma yake tunaweza kuongea nao huku akiwa na mkataba mwingine wa Simba.”
Kwa Msimu huu 2020/21, Onyango amekua chaguo la kwanza la Kocha Didier Gomes, huku akisaidiana na beki kutoka nchini Ivory Coast Pascal Wawa, na ikitokea hachezi basi asilimia kubwa huwa na sababu za kuwa majeruhi ama matatizo binafsi.