Shirika la viwango Tanzania (TBS), limetoa wito kwa taasisi za serikali na binafsi kutumia huduma za maabara zilizopata cheti cha ithibati ya umahiri na huduma zinazotolewa TBS ili kupata uelewa wa kitaalamu kwenye masuala ya utengenezaji na utekelezaji wa viwango vya ithibati.
Viwango vinavyotumika ni pamoja na 17025 ambacho kinatoa matakwa ya ithibati ya umahiri kwa ajili ya maabara ya upimaji na ugezi, ISO 15189 kinachotoa umahiri maabara za hospitali, ISO 17020 kwa ajili ya ukaguzi na ISO 17021 kwa ajili ya taasisi zinazofanya kaguzi za mifumo ya ubora.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 28, 2021, Afisa udhibiti ubora mwandamizi wa TBS, Stella Mloso amesema kuwa Ithibati ni utambulisho wa kitaalamu unaotolewa kwa taasisi na mamlaka ya ithibati ili kuthibitisha umahiri katika kutoa huduma husika, ambapo ithibati ya umahiri inatolewa kwenye taasisi zinazotoa huduma za upimaji kama maabara za hospitali, maabara za TBS, maabara zilizo katika vyuo vya elimu na utafiti maabara.
Amesema mfumo wa Ithibati unasaidia kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa nchi ambazo hutumia bidhaa zilizopitishwa kwenye maabara za ithibati na husaidia kuboreshwa utendaji kwa kutambua vihatarishi na kuviwekea mkakati wa kuvizuia.
Aidha, ameelezea ithibati ya Tanzania kuwa kuna maabara 42 ambazo zimepata ithibati ya umahiri ikiwa ni pamoja na maabara za upimaji vyakula, maji, kemikali, mafuta ya gari, vifaa vya ujenzi, umeme, vifaa vya uandisi na maabara za utamaduni.