Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amempongeza Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani kwa hatua alizozichukua za kuwasimamisha kazi wafanyakazi waliohusika na uzembe uliopelekea kituo cha kupoza umeme cha Msamvu kuungua moto na kusababisha adha kwa watumiaji wa huduma ya umeme kutoka katika kituo hicho.
Ameyasema hayo leo Agosti 14, 2021) alipotembelea kituo hicho ambacho kilipata hitilafu Agosti 2, 2021 ya kuungua kwa sehemu ya kituo hicho kinacho sambaza umeme katika Mkoa wa Morogoro na maeneo mengine Nchini.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa, amemuagiza Waziri Dkt. Kalemani kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaobainika kuhusika na kuungua kwa kituo hicho pindi uchunguzi wa tume aliyoiunda utakapokamilika.
Sambamba na hayo pia amewataka wataalam wanaosimamia vituo vya kupoza umeme nchini kuwa makini na kuzingatia weledi katika usimamiaji wa vituo hivyo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi na hasara kwa Serikali .
“Taarifa inaonesha kwamba kumbe ilisha onesha kuna hitilafu alafu mtu akalazimisha kuirudisha tena, ikaonesha tena ina shida na bado akarudisha tena, mtu huyo ni mtaalam na anajua tatizo la umeme na anajua hatari ya umeme, Ni bora umemsimamisha kwa sababu amefanya makusudi,” Amesema Majaliwa.