Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka viongozi wa maeneo mbalimbali nchini kuanzia ngazi ya kijiji kuhakikisha wanasimamia haki na amani ili kujiepusha na vitendo vya rushwa lakini pia kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga huku akiendelea kusisitiza uongozi wa Wilaya kutoa elimu zaidi kwenye jamii juu ya umuhimu wa makundi ya Wakulima na Wafugaji.

Hayo yamejiri baada ya Naibu Waziri Ulega kupokea taarifa ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji hadi kusababisha vifo vya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu ya mahusiano baina ya makundi hayo mawili.

“Kitendo cha ng’ombe kupelekwa kwenye mashamba ni jinai kama jinai nyingine siyo haki kwa mkulima au mfugaji kuchukua hatua kinyume na taratibu na viongozi wa kijiji wawe wasimamizi wa haki na amani na wasifanye upendeleo pamoja na kufanya vitendo vyovyote vya rushwa,” Amesema Naibu Ulega.

Aidha Ulega amesema wafugaji lazima waishi kwa upendo maeneo walipo pamoja na wafugaji wengine na wakulima kwa kuwa ni dhambi kubwa kuchukua mifugo na kuingiza kwa makusudi kwenye shamba la mkulima.

Halikadhalika Uongozi wa Wilaya umeiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inaweka mikakati mbalimbali ya kukomesha migogoro hiyo ambayo imekuwa ikisababisha hofu, ukizingatia Wilaya ya Handeni ina mifugo mingi na imekuwa ikifanya biashara ya kupeleka mifugo ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga (hawapo pichani) mara baada ya kufika katika wilaya hiyo kwa ziara ya kikazi ya siku moja, Mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga na kutoa maagizo ya kukomeshwa kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji kote nchini, mara baada ya kufika katika wilaya hiyo kwa ziara ya kikazi ya siku moja.

Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto afariki Dunia
Katibu mkuu wa CCM atoa pongezi kwa wakandarasi