Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, amekutana na Mabalozi,Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa yaliyopo hapa Nchini kwa lengo la kuwapa mrejesho kuhusu Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.
Akizungumza na Mabalozi hao, Waziri Mulamula amesema Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano uliofanyika Lilongwe Malawi 17 -18,Agosti,2021 kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kukabiliana na janga la UVIKO -19 ikiwa ni pamoja na kushawishi Kampuni zinazozalisha chanjo kutoa kibali ili teknolojia yao itumike kuzalisha chanjo hizo katika Nchi zinazoendelea kurahisha upatikanaji wa chanjo hiyo kwa wote na kwa bei nafuu.
Aidha kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mpango wa SADC wa kupeleka Jeshi katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji Balozi Mulamula amesema suala la ulinzi na usalama kwa nchi za SADC ni ulinzi na usalama kwa Tanzania,hivyo Tanzania imeshiriki kikamilifu kwa kutoa mchango wake wa fedha pamoja na jeshi.
Katika hatua nyingine Balozi Mulamula ametoa angalizo kwa Mabalozi wanaokwenda Mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Freeman Mbowe kufuata sheria na taratibu za Kimataifa kuhusu masuala ya Kidiplomasia ili kujiepusha na ukiukwaji wa sheria na taratibu.
Aidha Balozi Mulamula amefafanua kuwa Serikali haina lengo la kuwazuia Mabalozi hao kwenda Mahakamani kufuatilia kesi hiyo, bali kutokana na na uwepo wa janga la UVIKO -19 pamoja na msongamano ni muhimu kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufuatilia shauri hilo kwa njia nyingine ikiwemo kupitia vyombo vya habari.
Amesisitiza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndio yenye jukumu la kuhakikisha usalama wa Wanadiplomasia waliopo hapa nchini.
Hata hivyo,kwa siku za hivi karibuni baadhi ya Wanadiploamasia hao wameonekana Mahakamani bila kufuata sheria,kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya Kidiplomasia ikiwemo kutoa taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Katika Mkutano huo baadhi ya Mabalozi wamepongeza mafanikio yaliyopatikana na kueleza kuridhishwa na namna Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inavyoendesha shughuli zake pamoja na namna inavyotatua changamoto mbalimbali.