Uongozi wa klabu ya Young Africans umethibitisha kuwakosa wachezaji wao watatu ambao hawataruhusiwa kucheza mchezo wa Mkondo wa kwanza hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Rivers united ya Nigeria.

Young Africans itakua mwenyeji wa Rivers United, Jumapili (Septamba 12) katika Uwanja wa Benjamin Makapa jijini Dar es salaam, kuanzia mishale ya saa kumi na moja jioni.

Msemaji wa Klabu hiyo Haji Sunday Manara amezungumza na waandishi wa habari leo mchana na kuthibitisha taarifa hizo, lakini akawatoa wasiwasi Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kwa kuwaambia Ushindi utapatikana Jumapili kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Manara amesema sababu kubwa ya kuwakosa wachezaji hao kwenye mchezo dhidi ya Rivers United, ni kufuatia vibali vyao vya uhamisho wa kimataifa (ITC) kushindwa kuwasili kwa wakati kama ilivyokua inatarajiwa, kutoka kwenye vilabu walivyokua wakivitumikia kabla ya kujiunga na Young Africans mwezi uliopita.

“Tutawakosa wachezaji wetu Khalid Aucho, Fiston Mayele na Djuma Shabani kuelekea mchezo wetu dhidi ya Rivers United kutokana na ITC zao kuchelewa, kiukweli ni pengo hatuwezi kusema sio pengo ila ondoeni hofu tumesajili wachezaji bora wengi”

“Mpaka sasa hatujapata idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia uwanjani, tunasubiri taarifa ya CAF kupitia TFF ndani ya saa 24 tunaweza kuipata ndio maana hatujatangaza viingilio kwanza”

“Kesho nitakutana na vikundi vya hamasa. Hatuendi uwanjani kukaa, tunatakiwa kuanikiza na kuwapa nguvu wachezaji muda wote. Nilikuwa naona wivu sana wenzangu mlikuwa mnatumia nguvu kidogo tu uwanja unajaa, mimi ilibidi nitumie nguvu nyingi sana”

“Malengo yetu sio kufika tu ‘Group Stage’ ni kuvuka na kufika mbali zaidi. Sisi ndio mabingwa na ndio timu ya kwanza Tanzania kufika Group Stage na Quarter Final kwenye Ligi ya Mabingwa na Slogan tunayokwenda nayo ni The Return Of Champions” amesema Haji Manara.

Young Africans imepata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya Tanzania kufikia viwango vya kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa na kuthibitishwa na Shirikisho la soka Barani Afrika CAF.

Msimu uliopita Young Africans ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakitanguliwa na Mabingwa Simba SC, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Azam FC na Biashara United ilimaliza nafasi ya nne, na zote kwa pamoja zitashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho.

Simba SC yaanika mipango ya 2021/22
Waziri Bashungwa aipongeza Taifa Stars