Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Simba SC Hassan Dalali ameutaka Uongozi wa klabu hiyo kutoa nafasi kwa Wazee ili wazungumze na Wachezaji kuelekea mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo Jumapili (April 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kucheza mchezo wa Mkondo wa pili Afrika Kusini Jumapili (April 24).
Dalali ametoa ombi hilo kwa Uongozi wa Simba SC alipozungumza na Wanachama katika hafla maalum ya uzinduzi wa Kampeni ya Uhamasishaji iliyofanyika Maduka Mawili-Chang’ombe jijini Dar es salaam.
“Wachezaji wanapaswa kufahamu umuhimu wa mchezo huu, ikiwezekana Uongozi utupe nafasi sisi wazee tuzungumze nao, na kama itashindikana nipeni mimi pekee yangu nikazungume nao.”
“Wachezaji wengine wanakua hawajui Wanachama/Mashabiki wanaumia namna gani, watu wanakufa kwa ajili ya timu yao, kwa mfano tukifungwa unakua mchezaji anaweka Headphones anakula mziki wa Ally Kiba, anapaswa kuhisi uchungu wa kupoteza, tupeni wazee tuzungumza na hawa vijana.”
“Wanapaswa kufahamu kwa nini Simba ilianzishwa, kwa nini watu wanakufa kwa ajili ya Simba, Kwa nini wanawake wanapewa talaka kwa ajili ya Simba, nadhani tukiwapa vijana maneno mazuri, naamini hatoki mtu pale.” amesema Dalali
Simba SC ilitinga Robo Fainali kwa kishindo kwa kuichapa USGN ya Niger mabao 4-0 kwenye mchezo wa Hatua ya Makundi, ikimaliza nafasi ya pili kwa kufikisha alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco.