Umoja wa Mataifa umefaya tukio maalum katika ukumbi wa Baraza Kuu, Makao Makuu ya Umoja huo jijini New York Marekani ambapo Rais wa Baraza hilo, Abdulla Shahid, ameangazia maisha ya Mandela kama mtu mtafutaji wa haki asiyechoka wa “usawa na uhuru kwa wote”.
Shahid ametumia maneno ya Hayati Madiba na kusisitiza kuwa, “hakuna mtu anayezaliwa akimchukia mtu mwingine kwa sababu ya rangi ya ngozi yake, asili yake au dini yake” na akasisitiza zaidi kuwa vita yake ilikuwa ni kwa ajili ya utu wa watu wote.
Amesema, Wakati wa mtikisiko, maisha ya Madiba yanafundisha kuchagua utu badala ya kudhalilisha, kupaza sauti wakati wa dhuluma, na kusamehe badala ya chuki na kwamba ameacha ushuhuda wa utatuzi endelevu wa migogoro unaohitaji kukomesha ghasia.
“Na hii inategemea haki na huruma, kama ilivyowekwa wazi na Tume ya Ukweli na Upatanisho ambayo iliundwa nchini Afrika Kusini ili kukuza upatanisho na msamaha kati ya wahalifu na waathiriwa wa ubaguzi wa rangi,” ameongeza Shahid.
Katika mjadala huo, walikuwepo mjukuu wa Malkia Prince Harry, mjukuu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza kushiriki hafla ya Baraza Kuu ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya Nelson Mandela, na wakatumia sehemu ya hotuba yao kulaani kwamba “tunashuhudia shambulio la kimataifa dhidi ya demokrasia na uhuru, jambo ambalo Mandela alijitolea maisha yake.”
Prince Harry ambaye ameambatana na mkewe, Meghan amesema tunaishi katika “wakati muhimu” ambapo majanga mengi yanayobadilika, kama vile Uvikoid-19, mabadiliko ya tabianchi na habari potofu, ambayo yamesababisha mambo yasiyo na mwisho katika dhuluma inayowaumiza watu wa chini.
“Maamuzi haya yanaweza yasiendane na ajenda za vyama vyote vya siasa. Wanaweza kuamsha upinzani kutokana na masilahi yenye nguvu. Lakini nini cha kufanya haina mjadala. Na wala sio sayansi. Swali pekee ni iwapo tutakuwa wajasiri wa kutosha na wenye hekima ya kutosha kufanya kile kinachohitajika,” Amesisitiza Prince Harry.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, akihutubia hafla hiyo ametoa wito kwa kila mtu kuheshimu urithi wa Nelson Mandela kwa kuchukua hatua mfanano ili kusaidia kuleta amani na utulivu wa mataifa.
Amesema, “leo na kila siku, tuheshimu urithi wa Nelson Mandela kwa kuchukua hatua. Kwa kupaza sauti dhidi ya chuki na kutetea haki za binadamu. Kwa kukumbatia ubinadamu wetu wa kawaida, matajiri katika utofauti, sawa kwa heshima, umoja katika mshikamano. Na kwa pamoja kuifanya dunia yetu kuwa ya haki zaidi, yenye huruma, yenye mafanikio, na endelevu kwa wote.”