Wanasayansi wanasema spishi ya mbu vamizi huenda ndio waliohusika na mlipuko mkubwa wa malaria nchini Ethiopia mapema mwaka huu, matokeo ambayo ni ishara ya kutia wasiwasi kwamba maendeleo ya utafiti dhidi ya ugonjwa huo, yako hatarini kusambaratika.
Mbu aina ya Anopheles stephensi, ameonekana zaidi nchini India na Ghuba ya Uajemi na mwaka 2012, iligunduliwa nchini Djibouti na tangu wakati huo imepatikana katika Sudan, Somalia, Yemen na Nigeria.
Mbu hao, wanashukiwa kuchangia kuongezeka kwa ugonjwa wa malaria hivi karibuni nchini Djibouti, na kusababisha Shirika la Afya Duniani, WHO kujaribu kuzuia wadudu hao kuenea zaidi barani Afrika.
Siku ya Jumanne (Novemba 1, 2022), mwanasayansi wa malaria, Fitsum Tadesse aliwasilisha utafiti katika mkutano wa Jumuiya ya Madawa ya Kitropiki ya Marekani huko Seattle, na kusema mbu vamizi pia walihusika na mlipuko nchini Ethiopia.
Maafisa wa afya katika eneo la Dire Dawa, katika kituo kikuu cha usafirishaji waliripoti kuongezeka kwa kasi kwa ugonjwa wa malaria huku mwanasayansi mkuu katika Taasisi ya Utafiti ya Armauer Hansen huko Addis Ababa, Tadesse akiungana na timu hiyo ya uchunguzi.
Watafiti hao wanafuatilia zaidi ya visa 200 vya malaria, kuchunguza maeneo ya karibu ya mbu na kupima mbu vamizi kwa vimelea vya malaria huku wakibainisha kuwa ugonjwa wa malaria unaoenea zaidi barani Afrika umekuwa ukienea maeneo ya vijijini, kutokana na mbu wa asili kutopenda kuzaliana katika miji iliyochafuliwa.