Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka maafisa wa maendeleo ya jamii kwenda na kasi, ili kuchochea maendeleo ya jamii ikiwemo utekelezaji wa sera, mikakati, sheria na miongozo wakati Serikali ikiendelea kufanyia kazi changamoto za upungufu wa watumishi, mazingira ya kazi na sheria ya taaluma.
Waziri Gwajima, ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Mkutano wa Mwaka wa kada hiyo cha Maafisa wa Sekretarieti za Mikoa na Wakuu wa Idara za Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na kusema Serikali ina matumaini makubwa na mchango wa kada hiyo na itahakikisha inafanya uwezeshaji, Ili kwenda na kasi iliyokusudiwa.
Amesema, “Rais Samia Suluhu Hassan anatambua umuhimu wa sekta ya Maendeleo ya Jamii katika kuiwezesha Jamii kushiriki kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali walizonazo na ndiyo maana amechukua hatua ya kuunda wizara mama ya sekta hii na mambo mengi mazuri yanakuja.”
Dkt. Gwajima, pia ameeleza umuhimu wa kada ya maendeleo ya jamii na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwezesha mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto, huku akirejea mpango kazi wa Taifa wa kupambana na ukatili akisema serikali inakamilisha ya utekelezaji wa miaka mitano iliyopita ili kuja na mpango mpya ambao utkaojibu mahitaji ya sasa kwenye mapambano.
Hata hivyo, amewakumbusha Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhusu kusimamia masuala yanayotekelezwa na Serikali ambayo ni majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, utekelezaji wa ahadi za nchi kupitia Jukwaa la kizazi chenye usawa ambapo Tanzani ni kinara wa eneo la haki na usawa wa kiuchumi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amewataka Maafisa hao kutimiza majukumu yao kulingana na mipango iliyowekwa na sheria zilizopo na kusema, “Maafisa Maendeleo ya Jamii, muda wa kuambiana umepita kila mmoja asimame vema Fanyeni kazi na Wadau. Kila mnachopanga Mpange na Wadau.”
Naye, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Naibu Katibu Mkuu Ramadhami Kailima amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii ndio Wasimamizi na Watekelezaji na amewahimiza watumie Mikutano ya Mkoa na Wilaya, kuzungumzia Majukumu yao.