Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko leo Desemba 28 amepokea vyumba 51 vya madarasa yaliyokamilika katika Manispaa ya Mpanda, ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa ajili ya muhula mpya wa masomo 2023.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyumba hivyo 51 vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lyamba Manispaa ya Mpanda, Mrindoko ameipongeza Manispaa ya Mpanda kwa kukamilisha Ujenzi huo kwa wakati.
Amesema, Viongozi wa ngazi zote ndani ya Manispaa ya Mpanda na Mkoa wa Katavi wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha wanafunzi wote 14,904 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023, wanaripoti shuleni mapema ifikapo Januari 9, 2023.
Katika hatua nyingine, Mrindoko amewataka viongozi wa kijamii mkoani Katavi kuhakikisha wanatoa hamasa ya kufanya maandalizi ya watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa wakati, badala ya kusubiri mpaka shule zifunguliwe na kusisitiza kuwa hatosita kuchukua hatua za kisheria kwa yoyote atakayechelewesha mtoto kuripoti.
Akiwasilisha taarifa katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli amesema ujenzi wa vyumba 51 vya madarasa ndani ya Manispaa hiyo ulianza Oktoba 2022, ambapo walipokea Fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1 nje ya ukomo wa bajeti kwa ajili ya maandalizi ya mapokezi ya Wanafunzi wa Kidato cha kwanza.