Umoja wa Ulaya umeitaka Rwanda kuacha kuunga mkono kundi la waasi la M23, ambalo limeteka maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidekrasia ya Kongo .
DRC, Marekani na nchi kadhaa za Ulaya mara kwa mara imekuwa ikishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kikosi cha M23, ingawa Kigali inakanusha mashtaka hayo.
Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema Umoja wa Ulaya umeitaka Rwanda iache kuwaunga mkono M23 na kutumia njia zote kuwashinikiza waasi hao kufuata maamuzi yaliyochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Maoni ya Borrell yanakuja baada ya ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu DRC kuashiria kuwa imekusanya uthibitisho wa kuingilia moja kwa moja kwa vikosi vya ulinzi vya Rwanda ndani ya ardhi ya DRC kati ya Novemba 2021 na Oktoba 2022.
Katika taarifa yake Kinshasa ilikaribisha matokeo ya wataalam wa Umoja wa Mataifa lakini ilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchunguza ripoti ya wataalam kwa lengo la uwezekano wa vikwazo dhidi ya Rwanda.
Wakati huo huo, Rais wa Rwanda Paul Kagame aliilaumu Kinshasa kwa machafuko katika maeneo yake ya mashariki yenye hali tete katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya.
“Baada ya kutumia makumi ya mabilioni ya dola katika ulinzi wa amani katika miongo miwili iliyopita, hali ya usalama Mashariki mwa Kongo ni mbaya zaidi kuliko hapo awali,” Kagame alisema katika taarifa yake Jumamosi.
“Ili kuelezea kushindwa huku, baadhi ya jumuiya ya kimataifa wanailaumu Rwanda, ingawa wanajua vyema kwamba jukumu la kweli ni la serikali ya DRC. Ni wakati mwafaka ambapo udhalilishaji usio na msingi wa Rwanda ukomeshwe.” ameeleza.