Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF, Bunju kitatatua changamoto ya Watanzania kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa kufata huduma hizo.

Dkt. Mwinyi ameyabainisha hayo hii leo Fbruari 6, 2023 Jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF, kilichopo Bunju jijini Dar Es Salaam na kuongeza kuwa baadhi ya Watanzania walilazimika kutafuta huduma za upandikiza mimba nje ya nchi na kwa gharama kubwa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Amesema, “ni dhahiri wananchi wachache tu wenye uwezo ndio wanaomudu lakini walio wengi wanashindwa kupata huduma hizi ushahidi wa dhamira na jitihada za taasisi hii za kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za afya zinazotolewa hapa Tanzania jambo ambalo lilikuwa harakati za Hayati Dkt Kairuki enzi za uhai wake.”

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema afya ya uzazi ni jambo ambalo Hayati Prof. Kairuki aliliwekea uzito na huenda alifanya hivyo kutokana na changamoto inayowakabili kina mama kutopata ujauzito na huku akimshukuru Mwenyekiti wa Taasisi ya Afya na Elimu, mama Kairuki kkwa kumualika kwenye ufunguzi wa kituo cha Kairuki Green IVF na kumbukumbu ya Hayati Prof. Kairuki.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia), akipokea maelekezo wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Sekta binafsi katika kuhakikisha wanatatua tatizo la ugumba nchini ili wananchi wapate huduma bora za matibabu hayo na kudai kuwa tatizo la ugumba nchini linaanzia asilimia 30 mpaka asilimia 80.

“Natambua ukubwa wa tatizo hili na sisi wenyewe kama Serikali hatuna hata kituo kimoja cha kutoa huduma hizo, Wizara ya Afya tutaendelea kushirikiana na Kairuki Green IVF kuhakikisha kwamba wanawafikia Watanzania wengi, ili kutoa huduma bora za matibabu,” amesema Waziri Ummy.

Sitaangalia nafasi ya mtu suala la ulipaji kodi: Ruto
Watano wafariki kwa homa ya uti wa mgongo, maambukizi 37