Jeshi la Polisi Nchini, limetoa wito kwa Watendaji na Askari Kata kushirikiana kwa pamoja
kupinga na kukemea vitendo vya kihalifu, hasa vile vya ukatili wa Kijinsia ambavyo vimekuwa vikitukia au kuripotiwa katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Polisi Jamii Nchini, Faustine Shilogile wakati akizungumza na Watendaji wa Kata pamoja na Wakaguzi wa Kata za Jiji la Arusha, tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji.
Shilogile amesema, watendaji hao wanatakiwa kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusiana na madhara ya uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekua vikiongezeka katika jamii kila uchao.
Kuhusu eneo la utalii Shilogile pia amewataka Viongozi hao kutambua wajibu walionao wa kuhakikisha watalii wanaofika katika jiji hilo wanakua salama wakati wote na kuwataka kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vitaimarisha usalama.