Serikali imewataka Wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini, kuzingatia Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira zilizoanishwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi Mazingira(NEMC) wakati wa uanzishaji, uendelezaji wa viwanda nchini.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu sekta ya mazingira aliyoifanya katika viwanda vya Multi Cable Ltd na Nyakato Steel Mills Ltd vilivyopo Wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza.
Amesema, dhamira ya Serikali ni kuinua uchumi wa viwanda ili kuweza kukuza Pato la Taifa, kukuza wigo wa ajira kwa vijana na kutengeneza uhusiano mzuri baina ya Serikali na wawekezaji, hivyo yapo masuala muhimu ya kimazingira yanayopaswa kupewa kipaumbele na wawekezaji na wamiliki wa viwanda hivyo nchini.
Khamis ameyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na viwanda kutenga bajeti maalum, kwa ajili ya shughuli za mazingira katika jamii inayozunguza mradi wa uwekezaji ambapo wamiliki hawana budi kusaidia vifaa muhimu vinavyosaidia usafi wa mazingira katika eneo husika.
Aidha, amesema jambo lingine muhimu ni pamoja kutenga bajeti maalum ya utunzaji na upandaji miti pamoja na Mpango Kabambe wa kubadiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili nchi na dunia kwa ujumla.
“Nimetembelea na kuona uzalishaji katika kiwanda cha Multicable kuna matumizi ya miti ya asili tuliyoipanda. Kwa tafsiri ya haraka hapa tumeharibu mazingira, nawakumbusha wamiliki kuwasiliana na Ofisi yetu ya NEMC ili kuweza kuingia katika teknolojia ya kisasa ya nishati mbadala,” amesema Naibu Waziri Khamis.
Naibu waziri huyo, pia aliwakumbusha wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini pia kuhakikisha wanadhibiti utilishaji wa majitaka kutoka viwandani kwenda katika makazi ya wananchi sambamba na kuiagiza NEMC Kanda ya Ziwa kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuona utekelezaji wa maagizo hayo aliyotatoa kwa wawekezaji na wamiliki wa viwanda hivyo.