Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania – TASAC, limejipanga kutekeleza mradi wa kujenga vituo vinne vya uokozi (search and rescue centres – SARs), maeneo ya Kanyala Sengerema, Musoma – Mara, Nansio – Ukerewe na Ilemela Mwanza.
Hayo yameelezwa hii leo Machi 7, 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Mkeyenge wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Shirika kwa mwaka 2021/2022/2023.
Amesema, mradi huo unaotekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda utagharimu kiasi cha Shilingi 59.23 Bilioni, ambapo upande wa Tanzania gharama za mradi ni Shilingi 19.97 Bilioni zikijumuisha gharama za kazi za ndani.
Vituo hivyo, vitasaidia kushughulikia changamoto za usafiri kwa njia maji na katika uokozi majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kwa njia maji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria.