Watu tisa wamefariki na wengine 30 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka katika Mlima Nkondwe uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, huku chanzo cha ajali hiyo kikiwa bado hakijajulikana.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame amesema ajali hiyo imetokea Machi 6, 2023, ikihusisha Basi hilo aina ya TATA, lenye namba za usajili T506 DHH mali ya kampuni ya Komba’s.

Ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya Komba’s na kuuwa watu tisa.

Amesema, “baada ya kufika katika Mlima huo gari liliserereka na kudondokea kwenye bonde kubwa lenye kina cha Mita zisizopungua 75, chanzo cha ajali bado hakijajulikana. Jeshi la Polisi inaendelea na uchunguzi huku zoezi la kuitambua miili likiendelea.”

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Dkt. Alex Mrema amesema watu hao tisa walifariki papohapo ambao ni Wanaume watano watatu wakiwa ni Watoto na Wanawake wanne akiwemo mjamzito.

Basi hilo mara baada ya kupata ajali. Picha ya The Katavi Independent.

Akisimulia tukio la ajali hiyo, mmoja wa majeruhi Philbert Focus amesema mara baada ya kufika kwenye kona ya mlima huo basi lilianza kwenda kwa kasi na hivyo kushindwa kukata kona na kupitiliza kwenda bondeni na kupinduka.

Aidha, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Hamad Kambi amesema, “mimi ndio nilikuwa wa kwanza kufika pale kiukweli ajali ilikuwa mbaya sana, lakini japo sikuwa na gloves lakini niliona wale ni binadamu wenzangu na niliwaokoa baadhi ya watu na kutoa maiti nne.”

Wanawake WCF wagharamia matibabu upasuaji wa moyo
Ukosefu wa maadili kaa lamoto, Wananchi wapaza sauti