Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Rufiji, Canute Msacky amethibitisha vifo vya watu saba waliopoteza maisha kwa kula Samaki aina ya kasa anayesadikiwa kuwa na sumu ambapo sita kati ya hao ni watoto.
Taarifa za vifo vya Watu hao saba zilianza kusambaa katika vyombo vya Habari hapo jana Machi 13, 2023, ambapo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bweni, Juma Khamis alisema watu wengine wanane walikuwa wakiendelea kupatiwa matibabu katika vituo vya afya, Mafia.
Kaimu Kamanda Msacky amesema Watu hao wanatoka kwenye kaya nne tofauti za kijiji hicho na walifariki kwa nyakati tofauti Machi 12, 2023 huku akiyataja majina yao kuwa ni Mohamed Makame (miezi 7), Minza Hatibu (miezi 10), Ally Seleman (miezi 8), Ramadhan Karimu (miezi 8), Abdala Nyikombo (4), Makame Nyikombo (9) pamoja na Salima Mjohi (28).
Amesema, “ni kweli tukio lipo ni watoto sita wa kuanzia miezi saba na mtu mzima mmoja ndio wamefariki, na taarifa za awali ni kwamba wamekufa baada ya kula Samaki aina ya Kasa anayesadikika kuwa na sumu, na hawa watu walipoteza maisha kwa nyakati tofauti.”
Kuhusu chanzo cha tukio hilo, Kaimu Kamanda Msacky amesema wanawashikilia watuhumiwa watatu kwa mahojiano, na kwamba uchunguzi juu ya tukio hilo bado unaendelea huku likiwataka Wavuvi kuacha tabia ya kuvua nyara za Serikali.