Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano ya Kimataifa ngazi ya Vilabu, Simba SC na Young Africans watacheza mwishoni mwa juma hili katika viwanja vya ugenini nchini Morocco na DR Congo kwa ajili ya kuhitimisha Hatua ya Makundi, huku tayari wakiwa na tiketi ya Robo Fainali ya michuano hiyo.
Simba SC yenye alama 09 katika kundi ‘C’ Ligi ya Mabingwa Barani Afrika itacheza na vinara wa kundi hilo Raja Casablanca Aprili Mosi nchini Morocco, huku Young Africans itacheza dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika Aprili 2.
Mchezo wa Simba SC dhidi ya Raja Casablanca ambao umpengwa kuanza saa nn usiku kwa saa za Morocco sawa na saa Saba usiku kwa saa za Afrika Mashariki, utachezeshwa na Mwamuzi Ahmad Heeralall kutoka Mauritania.
Mchezo wa Young Africans dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki mjini Lubumbashi-DR Congo, utachezezwa na Mwamuzi Lahlou Benbraham wa Algeria.
Rekodi zinaonyesha katika michezo 13 ya Kimataifa aliyochezesha mwamuzi, Ahmad Heeralall ni mchezo mmoja tu ambayo hajatoa kadi ya njano huku nyekundu ikiwa ni moja.
Katika michezo hiyo timu za nyumbani zimeshinda michezo minane, sare minne huku ya ugenini ikishinda mmoja tu ambao ulikuwa wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi ambapo Young Africans ilipoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Julai 29, 2018.
Kwa Young Africans, Lahlou amechezesha michezo 10 ambapo ametoa kadi za njano 31 na nyekundu moja tu. Kwenye michezo hiyo 10 aliyochezesha timu zilizocheza nyumbani zimeshinda mitano, sare miwili huku zile za ugenini zikishinda michezo mitatu tu.