Tanzania imeungana na Afrika Kusini kuadhimisha Siku ya Afrika Mei 25, 2023 manispaa ya Mogala nchini Afrika Kusini kusherehekea miaka 60 ya Umoja wa Afrika tangu kuanzishwa kwake Mei 25, 1963 Addis Ababa Ethiopia.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema Siku ya Afrika ni siku muhimu ya kuwakumbuka viongozi walitoa mchango mkubwa wa kuzikomboa nchi za Afrika na jinsi walivyojitolea kuhakikisha Afrika inasonga mbele na kufika hapo ilipo na Zaidi.
Balozi Milanzi amesema, Tanzania imeshiriki katika sherehe hizo kwa kutuma ujumbe kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saidi Yakubu pamoja na kikundi cha Sanaa cha Safi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema siku hiyo ni adhimu kwa Afrika nzima, Watanzania wanawajibu wa kujivuania kuwa nchi yao ni miongoni mwa nchi waasisi wa umoja huo.
Amesema, Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ni miongoni mwa Viongozi waanzilishi wa Umoja huo na kuongeza kuwa ujumbe anaouongoza yupo pia Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab.
Akihutubia mamia ya wananchi wa Afrika Kusini pamoja na mabalozi wanawakilisha nchi zao nchini humo, Rais Cyril Ramaphosa amesema waafrika wanajivuvia historia yao na kujipanga kutengeneza kesho ya Waafrika wenyewe licha ya changamoto mbalimbali.
Amesema Changamoto hizo zinazokuzimba nchi za Afrika nyingi zinatatuliwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizo kwa njia ya kutoa wataalamu, ujuzi na kusisitiza kuwa Afrika ina wataalamu bora duniani wenye ujuzi katika fani mbalimbali.Siku ya Afrika imesherehekewa Afrika Kusini kwa kupambwa na bendera zote za nchi 54 za Afrika na kuhudhuriwa na mabalozi wa nchi 14 pamoja na viongozi mbalimbali.