Wangoni, ni moja ya kabila linalopaikana nchini Tanzania na sehemu zingine za kusini mwa bara la Afrika na kutokana na historia ya kabila hili kuonesha kuwa walipita sehemu mbalimbali wakitokea kusini mwa Afrika mpaka Afrika ya kati na mashariki, kuna mengi ya kujifunza juu yao.

Kiuhalisia kuna aina mbili za Wangoni, 1. Wangoni asilia na 2. Wangoni waliopenda tu kujipachika kwenye Kabila hilo, ila Wangoni wa asili ni wale ambao chimbuko lako ni kusini mwa Afrika.

Wangoni wa kujiita

Hawa ni wale wakazi waliokutwa kwenye maeneo yao na kuamua kujiita Wangoni kwa sababu mbalimbali ambazo wao walikuwa nazo(nitafafua hili kwa kina hapa chini). Kwa ujumla Yapo mengi sana ya kusimulia juu ya kabila hili la Wangoni. Ila kwa leo tutajadili mgawanyiko wa majina ya Wangoni.

Wengi tumekuwa tukifahamu kuwa Wangoni wanapatikana mkoani Ruvuma hasa kwenye wilaya ya Songea. Na kutokana na kabila hili kuwa kubwa na kuwa na uwezo wa kutawala sehemu hizo imekuwa ni kama wao ndio wakazi asilia wa Songea na baadhi ya sehemu ya mkoa wa Ruvuma.

Lakini uhalisia ni kwamba, kulikuwa na wakazi waliopata kuishi hapo hata kabla ya ujio wa Wangoni kwenye ardhi ya Ruvuma. Kwa mfano kulikuwa na makabila kama Wandendeule, Wayao, Wanyanja, Wamatengo na Wanindi.

Lakini kwa kuwa makabila haya yalikuwa hayana nguvu kivita, yakajikuta yakiwa chini ya kabila la Wangoni. Hivyo wapo waliokubali kutumia majina ya Wangoni ili kuleta heshima na wapo waliokataa kujiita majina ya Wangoni kama sehemu ya kupinga uwepo wao.

Wangoni waliuopenda Ungoni

Kulikuwa na Mngoni mmoja aliyefahamika kwa Jina la Mtepa Gama. Alisifika kwa mapambano na kuteka baadhi ya makabila. Sasa wale waliotekwa waliamua kujiita na wao Mtepa ili kuonekana kuwa wao ni ukoo mmoja na Mtepa Gama.

Na mateka hao walipozaliana watoto wao waliamua kuwapa majina ya Gama wakiona ni fahari na wakisema watoto hao ni mali ya Mtepa Gama na wakahesabika kama ukoo wa Mtepa Gama hali iliyopelekea kujikuta wanajenga ukoo ambao una jina la waanzilishi na ndio hao Wangoni walioupenda Ungoni.

Wangoni wa asili

Hawa majina yao walikuwa wanayarithii kutoka familia hadi familia na kutoka ukoo hadi ukoo ambapo sababu za wao kujiita majina hayo yanafahamika waziwazi tofauti na wale Wangoni waliokuwa wanajiita kwa sababu za kiutawala.

Kwa ujumla tunaweza kuyagawa majina ya wangoni katika mkundi yafuatayo. Na mgawanyiko wa majina haya yalitegemea sehemu walizokuwa wanafika na kuanzisha maisha yao huko.

i. Wangoni Waswazi: Walipata majina yao wakiwa kwenye ardhi ya Waswazi ambapo walizaliana na kukutana na wakazi wa hapo ndipo kukapatikana majina hayo. kwenye kundi hili kuna majina kama Gama, Tawete, Chingwe,Magagura,Mswami,Maseko,Nyumayo,Ole, Jere ,Mshanga,Masheula, Nkosi, Mlangeni Na Malindisa.

ii. Wangoni Watonga: Hawa ni wale waliopata majina yao wakiwa kwenye ardhi ya Watonga.na ndipo jina lao lilipobadilishwa kutoka Wanguni na Wangoni. Kuna majina kama, Makukura,Silengi,Ntocheni, Sisa, Ntani, Ngairo,Nguo, Matinga,Nkuna,Gomo na Pili.

iii. Wangoni Wasenga: Hawa waliopata majina yao wakiwa maeneo ya mto Zambezi mpaka kufikia maeneo ya Malawi. Kwenye kundi hili kuna majina kama,Lungu, Tembo, Njovu, Nguruwe,Ng’ombe, Mumba Na Mwanja.

iv. Wangoni Wakalanga: Wangoni hawa walipata majina wakiwa kwenye ardhi ya Wakalanga. Kwenye kundi hili kuna majina kama Mbano, Soko, Moyo,Zenda,Newa, Shonga, Shawa, Chiwambo, Hara, Mapara, Mteka Na Nyati.

v. Wangoni Wasukuma. Ni wale waliopata majina yao wakiwa usukumani na unyamwezi.hawa walipewa jina moja ya Watuta. Kwenye kundi hili kuna majina kama.Chisi, Ntara,Mpepo, Satu,Zinyungu, Chawa Na Mzila.

Shujaa wa kabila la wangoni, Nduna Songea Mbano.

vi. Wangoni Wandendeule: Ni Wangoni waliopata majina wakiwa kwenye ardhi ya Songea. Kwenye kundi hili kuna majina kama, Ngonyani, Mapunda,Ntini, Milinga,Nyoni,Henjewele,Ponera,Luhuwa, Nungu,Mango, Nyimbo, Humbaro,Kigombe, Wonde, Ndomba, Tindwa, Maginga na Luambano.

vii. Wangoni Wamatengo: Ni wale waliochanganyika na kabila la Wamatengo waliowakuta hapo Songea: kwenye kundi hili kuna majina kama, Nchimbi,Ndunguru,Komba,Nyoni, Kapinga, Kifaru, Pilika, Hyera, Mbele,Mkwera, Ndimbo, Mapunda, Ngongi, Mbunda, Kinyero,Nombo na Kumburu.

viii: Wangoni Wapangwa: Waliopata majina kutokana na kujichanganya na Wapangwa waliokuw wanapatika hapo Songea kabla ya Wangoni kufika. Kwenye kundi hili kuna majina kama, Mhagama,Kimhwili, Nditi, Kugongo,Njombi, Mwingira,Kihaule, Mbawala, Njerekela, Komba, Kayombo, Luena,Mbena,Mwagu, Mlimara, Sanga, Kokowo,Miloha, Kihuru, Chali Mwinuka, Nyilili, Mkuwa, Mhonyo, Mkinga, Ngoponda na Goliyama.

Ilikuwaje wakaitwa Wangoni

Asili ya jina la Wangoni linaanzia kusini mwa Afrika, ambako hapo awali kulikuwa na wakazi wengi katika koo za Wazulu waliofahamika kwa jina la Abanguni (kwa Kiswahili tunaweza kusema Wanguni) walioishi kusini mwa Afrika.

Kwa kipindi chote wakazi wote walikuwa wakifahamika kwa jina moja la Wanguni isipokuwa wale Khoisani na kwa miaka yote hiyo waliishi sehemu moja tu na hakukuwa na uhamiaji wowote nje ya ardhi ya Wanguni. Lakini baadaye eneo lao likaingiliwa na wageni, Wadachi. Na miaka ilivyozidi kwenda kuja wageni wengine, Waingereza.

Kutokana na maslahi ya kiuchumi, kidini na kisiasa kulisababisha wageni hao kupigana na kuongeza migogoro mikubwakusini mwa Afrika, ambayo kimsingi iliathiri sana jamii za Kiafrika, Wanguni wakiwemo.

Migogoro hiyo ikasababisha vita vya Mfekane miaka ya mwanzo ya 1800. Na vita hivyo vikasababisha baadhi ya Koo za Kinguni zilizokuwa kwenye makundi makubwa kuhama na kuelekea Afrika Mashariki na Kati. Wakati koo hizo zinatoka huko zilikuwa zikifahamika kama Wanguni.

Lakini mambo yalikuwa yakibadilika kadri walivyosonga, hasa maeneo waliyopita, mfano wakati Zwangendaba na Zwinde wanafika kwenye ardhi ya Wathonga maeneo ya Swaziland, Wathonga waliwaita Wangoni badala ya Wanguni.

Wao walitoa “U” na kuweka “O” kulingana na sheria na utaratibu wa lughu yao. Na hapo ndipo mabadiliko yalivyoanza kutokea katika zile koo maarufu, kutoka Wanguni hadi kuwa Wangoni.

Askari wa Kijerumani huko Songea.

Walipofika Nyasa kwenye miaka ya 1840/1850, walikuta makabila mengi sana, ila yaliyofahamika sana kutokana na biashara ni Wayao, ambao walihamia hapo baada ya kukimbia adha ya biashara ya utumwa iliyofanywa na Wamakua huko Msumbiji.

Hivyo kwa Wayao, Wangoni waliitwa Wagwangwala wakiwa na maana ya watu wenye haraka, na hii ni kutokana na mwonekano wa Wangoni kwenye ardhi ya Wayao, wakiwa wanatembea kwa haraka kuelekea maeneo mengine.

Mpaka kufikia kwenye miaka ya 1860, Wangoni walifika kwenye ardhi ya Wahehe. Lakini kabla ya kufika kwa Wahehe, walishafika maeneo ya Wasangu na Wabena. Lakini kutokana na kabila la Wahehe kuwa na ulinzi mkubwa na pia kuwa na jeshi imara lenye uzalendo wa hali ya juu hawakuwa tayari kuona ardhi yao ikivamiwa na kukaliwa na wageni ambao hawajulikani walipotoka.

Kaburi la Songea Mbano, mtu ambaye alifanya mji huo kuitwa jina lake.

Wahehe wakaingia vitani na Wangoni na kuwatimua katika ardhi ya Uhehe. Na mara baada ya vita hii Wahehe waliwapa jina kwa kuwaita Wamapoma au Wapoma, wakiwa na maana ya wavamizi waliovamia ardhi ya Wahehe na kuanzisha mapigano kuanzia kwa Wabena pamoja na Wasangu.

Na mpaka kufikia miaka ya 1870, Wangoni wakafika ardhi ya Unyamwezi na Usukumani ambapo huko waliitwa Watuta hasa na makabila kama ya Wafipa waliokuwa na ufalme wao kwa wakati huo katika ukanda mkubwa ikiwemo maeneo ya Ziwa Tanganyika.

Usikose sehemu ya Pili, Jumamosi ijayo (Juni 17, 2023) tutaangazia vita kati ya Wangoni na Wamatengo.

Vifo watu 12, Wanamgambo ADF watupiwa lawama
Trump ashitakiwa kwa matumizi mabaya nyaraka za siri