Mbunge wa Kongwa Job Ndugai amesema Serikali inachangia kuuwa historia ya Kongwa na kuibeba Mazimbu Morogoro na kusema kitendo hicho hakina afya kwao.
Ndugai ametoa kauli hiyo mbele ya Katibu Mkuu CCM Daniel Chongolo ambapo amesema Wilaya ya Kongwa ndiyo iliyobeba dhamana kubwa Kwa nchi za kusini mwa Afrika kwani kila jambo likipangwa Kongwa isipokuwa watu kwa mapenzi yao wameitukuza Mazimbu.
Amesema kabla ya kuelekea Mazimbu, wapigania uhuru waliishi Kongwa, wakafanya mikakati ya uhuru katika nchi zao na walipoona wamejiweka sawa walianza kutafuta njia za kuwaandaa viongozi kwa kuwapa elimu ndipo wakaenda kujenga kituo cha mafunzo Morogoro katika eneo la Mazimbu.
“Hapa pameachwa kwa kuchoka, inatushangaza kila wakati wakija wageni wanapelekwa Mazimbu na huko kumetunzwa vizuri siyo sawa kabisa, hapa ndipo walijifunza kwa mtutu wa bunduki na vyuma vililindima hapa,” amesema Ndugai.
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amekiri kituo cha Kongwa kwamba kimesahaulika na nguvu kubwa imepelekwa Mazimbu ambapo amesema jambo hilo linamkera hata yeye kwani anajua fika kwamba Kongwa ndiyo iliyobeba zaidi historia.
“Ni kweli hata mimi nafahamu hili na ndiyo maana nilizuia mmoja wa mabalozi mwaka jana badala ya kumpeleka Morogoro nikaamua aje hapa,” amesema Chongolo.
Katibu Mkuu ameagiza Wizara ya Utamaduni na Michezo kusimamia maboresho ya kituo hicho ili kifanane na hadhi yake.
Itakumbukwa Kituo cha wapigania uhuru Kongwa kwa nyakati tofauti walikaa Marais wa zamani Samola Machel (Msumbiji) na Sam Nujoma wa Namibia ambao baadae wanatajwa kuwa walirudi kuwashukuru wananchi.