Takribani Wanafunzi 25 wa Shule ya Sekondari ya Mpondwe Lhubiriha, (zamani Peter Hunter SS), wameuawa kufuatia shambulizi linaloshukiwa kufanywa na wapiganaji wa Allied Democratic Forces – ADF, katika eneo la Kasese, lililopo magharibi mwa mpaka wa nchi ya Uganda na DRC.

Tukio hilo, limetokea baada ya wanamgambo hao kuvamia Shule hiyo ya kutwa na bweni, wakati Wanafunzi hao walipokuwa wamelala na miili yao ilipatikana katika boma la shule, huku wengi wao wakikutwa wamekatwa kwa vitu vyenye ncha kali.

Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi Uganda limepeleka vikosi vya kupambana na ugaidi na vikosi maalum katika shule hiyo, huku ikidaiwa kuwa waasi hao wa ADF pia waliwateka nyara wanafunzi kadhaa, kuiba vyakula na vitu mbalimbali, kabla ya kuvuka kurudi DRC.

Mmoja wa watumishi katika shule hiyo, ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema wakati wa tukio kulikuwa na Wanafunzi 50 na walionusurika ni watatu pekee, hivyo ikimaanisha kuwa zaidi ya wanafunzi 20 ndio waliotekwa nyara na wanamgambo hao wa ADF.

Hili linakuwa ni tukio la pili, kwa wanamgambo kushambulia eneo la Uganda kutoka DRC katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, kwani Desemba 2022 jeshi la Uganda liliwaua wapiganaji 11 wa ADF baada ya kuingia Uganda kutoka DRC.

TGNP yataka Wanawake wakumbukwe
Serikali yaonywa: Tumechangia damu bure msiwauzie wahitaji