Jumuiya za Kimataifa zimetakiwa kushirikiana na Serikali za Mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, kwa kuongeza nguvu zaidi ili kuweza kuutokomeza kabla ya Mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akitoa tamko la Tanzania kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwenye vikao vinavyoendelea vya Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa.
Amesema, “bado hakuna rasilimali za kutosha kupambana na TB, tunaendelea kuhimiza wadau wa Sekta ya Afya kuunganisha nguvu za pamoja na kuwekeza zaidi kwenye rasilimali, tafiti, teknolojia, vifaa na vifaatiba.”
Aidha, ameongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye watu wengi wenye maambukizi ya Kifua Kikuu ikichangia asilimia 87 ya ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani na kwamba Takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha Tanzania ilikuwa na watu 132,000 wanaogua ugonjwa wa kifua Kikuu.
“Tumepunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huu kwa asilimia 32 na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 55, Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa huo ikiwekeza nguvu kwenye utoaji wa matibabu pamoja na utoaji wa elimu ya afya, ili jamii iweze kufahamu ugonjwa huo mapema na kupata matibabu,” alisema Waziri Ummy.