Umoja wa Waandishi wa Habari Tanzania – UTPC, umezindua ofisi zake Jijini Dodoma pamoja na Mpango Mkakati wake wa mwaka 2023-2025 uliofanywa na Mgeni Rasmi, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozak.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo Rais wa – UTPC , Deogratius Nsokolo amesema nchi ya Sweden imekuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha tasnia ya habari nchi inaendelea kuimarika na moja kati ya mchango wao ni pamoja na vifaa vya kufanyia kazi vya kisasa kama komputa
Amesema, mpango mkakati wa UTPC ni kukuza uwezo wa kitaaluma wa wanahabari nchini, uhuru wa kupata taarifa na habari, kuhakikisha klabu za waandishi zinafanya kazi kwa ufanisi kwa kuweka mifumo mizuri na dhabiti ya usimamizi pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama wao na maslahi vinazingatiwa na UTPC kuwa na mifumo mizuri inayochangia shughuli zake zinakua kwa ubora zaidi.
“Tunafahamu jukumu letu muhimu kama waandishi wa habari ni kuleta mabadiliko chanya kwa jamii yetu, hasa kwa kuwa sekta ya habari ina jukumu kubwa katika kutoa habari za ukweli na kuijenga jamii yenye taarifa na maarifa ili iweze kufanya maamuzi sahihi,” amesema.
Kwa upande wa mwakilishi kutoka Serikalini, Zamaradi Kawawa amesema kuwa wizara ya habari mawasiliano na teknolojia ya habari inawapongeza UTPC kwa kuimarisha sekta muhimu ya habari nchini pamoja na kuwa taasisi ya kwanza ya sekta ya habari kuhamia Dodoma.
“Hii inaonyesha ni kwa namna gani mmekuwa tayari kuunga mkono juhudi na maelekezo mbalimbali ya serikali yetu, tunawakaribisha taasisi nyingine za sekta ya habari kuja Dodoma kwasababu hii ndio makao makuu ya serikali lakini vilevile naomba niwapongeze kwa hatua nzuri ya kuandaa mkakati mpya wa kuhakikisha kwamba unaipeleka UTPC kwenye hatua nyingine na nawashukuru pia wadau wote ambao wamewezesha UTPC kufikia hatua hii.”
Akiongea kwa niaba ya Viongozi wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Nchini, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mwanza, Edward Soko amesema UTPC ina msaada mkubwa kwa waandishi hivyo ni jukumu la kila mtu kuhakikisha inasimama vyema na kuweza kufikia malengo waliyo jiwekea.