Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mrida Mshote amewataka wafugaji wa Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha wanawapeleka watoto shule na kuachaana na ile dhana ya kuwafanya watoto kuwa wachungaji wa mifugo.

Kadhalika Mrida amewataka viongozi wa CCWT Mpwapwa kuhakikisha wanatafuta wanachama ambao watajisajili kwenye chama hicho ili kuwe na kanzi data sawa ambayo itasaidia kwenye utatuzi wa changamoto za wafugaji Wilayani hapo.

Mrida ameyasema hayo leo Januari 12 2024, katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, wakati akizungumza na wafugaji wa Wilaya hiyo.

Amesema,  viongozi wa CCWT wa Wilaya hiyo wawe na maono, kwani chama hicho cha wafugaji kwa sasa kinataka kuona wafugaji wanakuwa na maendeleo ikiwemo kusomesha watoto huku akisema lengo la chama hicho kwa sasa ni kwenda kubadilisha maisha ya wafugaji.

“Umuhimu wa kuwa kwenye chama kwanza tunapenda kuwaeleza kwamba Chama kimebadilika, tuna vijana wasomi ambao wanatuelekeza dunia inaendaje na sisi tunataka tuone wafugaji wanakuwa na maendeleo hatutaki kuona wafugaji wanakuwa na watoto ambao hawaendi shule tuende na dunia inavyotaka,” aliongeza Mrida.

“Haiwezekani mtu una ng’ombe 500 ambao ni thamani ya hela nyingi sana lakini unatembea kwa miguu hauli vizuri watoto hawasomi mafuta ya kupaka hakuna tunataka watoto wasome si kwaajili ya kupata ajira tu hapana, bali wawe na maarifa ya kuendesha maisha katika jamii zetu sisi wafugaji” alisema.

Kuhusu Wafugaji kutokopesheka kwenye benki, Mrida amesema kwa sasa chama kimeenda kutafuta benki washirika watakao wakopesha wafugaji kwajili ya kuharakisha maendeleo yao katika kununua mazao mifugo na kadhalika.

“Haiwezekani wavuvi wanakopeshwa na mabenki wananua meli za kwenda kutafuta vitu ziwani visivyoonekana halafu sisi ambao tuna mifugo inayonekana hatukopesheki hii haikubaliki ndio maana leo tumekuja hapa na watu wa benki wawape elimu na muweze kwenda kukopa kwa tija kwaajili ya kuongeza wigo wa ufugaji,” alisema.

Hata hivyo ameongeza kuwa, wao kama CCWT wanafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kurahisisha baadhi ya mambo ikiwemo upatikanaji wa masoko na Chanjo kimataifa ya mifugo.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 13, 2024
Michuano Safari Lager Cup kutimua vumbi Mbeya, Mwanza