Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto nyingi za Muungano.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema hayo bungeni jijini Dodoma Februari 9, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Najma Murtaza Giga aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kuhakikisha changamoto
za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hazileti madhara nchini na lini zitapatiwa ufumbuzi.
Akijibu swali hilo, Dkt. Jafo amesema SJMT na SMZ zimetengeneza utaratibu wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Muungano kupitia vikao vyake na kwamba Serikali hizo mbili ziliunda Kamati ya Pamoja ya kutatua changamoto za Muungano ambayo huundwa na wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano.
Waziri Jafo amefafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa Kamati ya Pamoja mwaka 2006 hoja 25 zimejadiliwa na kati ya hizo 22 tayari zimepatiwa na
kuondolewa kwenye hoja za Muungano.
Ameongeza kuwa, hoja mbili zilizobaki katika orodha hiyo zipo katika hatua za kupatiwa ufumbuzi kupitia kamati hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka SJMT na SMZ huku akisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zanzibar wana nia ya dhati ya kuzitafutia ufumbuzi hoja hizo mbili zilizobaki.