Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali amewataka maafisa tarafa na watendaji wa kata Mkoa wa Kigoma kuhakikisha wanakusanya mapato na kutatua migogoro ya wananchi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali.

Kali ameyasema hayo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye na kuwaasa viongozi hao kubadilika kiutendaji na kuwa mfano bora kwa jamii wanayoiongoza.

Amesema, “niwaombe sana, mafunzo mnayoyapewa, yaende yakawabadilishe tuwe daraja, tusimamie mapato yetu, makusanyo yetu, msiruhusu migogoro.”

Aliongeza kuwa, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata ni daraja kati ya wananchi na Serikali na hivyo hawana budi kufanya kazi kwa weledi na nguvu zote hususani kwenye utatuzi wa migogoro kama ya wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) kwenye maeneo waliopangiwa

Aidha, amewataka watendaji hao kuacha kuamua kesi kienyeji bali wafuate sheria na miongozo ilioyopo kwani katika baadhi ya maeneo Watendaji wa Kata wameshindwa kusuluhisha baadhi ya kesi kama mimba za wanafunzi kutokana na kushawishika kwa namna mbalimbali ikiwemo rushwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa, Ibrahim Minja amesema mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuwajengea uwezo na kuwakumbusha maadili ya utumishi wa Umma Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kama Viongozi wa ngazi za jamii na kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali.

Naye Mwamvita Lusomi, Mtendaji wa Kata ya Lusimi katika Manispaa ya Ujiji Kigoma ameipongeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuwapatiia mafunzo hayo na anayo imani kubwa kuwa yatawawezesha kutatua migogoro miongoni mwa jamii inayowazunguka lakini pia watafanya vizuri zaidi kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato ili kufikia azma ya Serikali.

Krunoslav Jurcic kocha mpya Pyramids FC
Makundi maalum yapewe kipaumbele ununuzi wa Umma - Dkt. Biteko