Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema jitihada inahitajika katika kutoa elimu ya magonjwa yasioambukiza pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha, mazoezi na kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya moyo.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa moyo ni muhimu wananchi kufuata njia za kujikinga zaidi ikiwemo kuacha ulevi uliyopindukia, uvutaji sigara, tabia bwete pamoja na uzito uliyopindukia.
Amesema, Watalaamu wa Afya, Wasomi, Wyombo vya Habari pamoja na Watunga sera wanatakiwa kushiriki katika utoaji elimu kuhusu masuala ya afya na kwamba tafiti zinapaswa kufanyika kwa kina ili kubaini visababishi zaidi vya magonjwa ya moyo kwa kupata taarifa zaidi juu ya taratibu za kijamii na tabia za kiutamaduni katika mambo mbalimbali yaliyozoeleka kufanyika barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema, Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo kama vile kuimarisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kufanya tafiti za afya za kimkakati ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wananchi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa adimu.
Amesema Taasisi ya Moyo ya jakaya Kikwete imeendelea kuimarika ambapo kwa sasa inafanya upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 800 kwa mwaka ikiwemo upausaji wa kufungua kifua (upasuaji mkubwa) ukilinganisha na wagonjwa 200 wakati ikianzishwa na kwamba zaidi ya wagonjwa laki mbili hutibiwa kwa mwaka huku zaidi ya 2400 wakitoa mataifa mengine.