Uongozi wa Shirikisho la Soka nchini Nigeria ‘NFF’ umepanga kukutana kwa dharura na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya nchi hiyo José Vítor dos Santos Peseiro, ili kufanya maamuzi ya mustakabali wa baadae.
Kocha Peseiro, aliifikisha Nigeria ‘Super Eagles’ katika mchezo wa Fainali wa ‘AFCON 2023’ kabla ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Wenyeji Ivory Coast juzi Jumapili (Februari 11), mjini Abidjan.
Mkataba wa kocha Peseiro umesaliwa na mwaka mmoja, lakini una kipengele cha kumuwezesha kusaini mkataba mpya, lakini kikao chake na Uongozi wa ‘NFF’ kitaamua mustakabali wa kubaki ama kuondoka.
Rais wa ‘NFF’ Ibrahim Gusau, ameviambia vyombo vya habari vya Nigeria kuwa, pamoja na kutarajia kukutana na kocha huyo kutoka nchini Ureno, bado wamefurahishwa na kazi yake nzuri ambayo ameifanya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ kwa kukifikisha kikosi cha Super Eagles kwenye hatua kuusogelea ubingwa.
Desemba 29, 2021, Peseiro mwenye umri wa miaka 63 alifikia makubaliano ya mdomo na Shirikisho la Soka la Nigeria ‘NFF’ ili kuchukua nafasi ya Gernot Rohr aliyekuwa Kocha Mkuu wa Super Eagles kwa wakati huo.
Mei 15, 2022, Peseiro alitangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu mpya, na alifanya kazi kubwa ya kuipeleka Nigeria kwenye Fainali za AFCON 2023 zilizofanyika nchini Ivory Coast.