Dhoruba wakati wa msimu wa mvua si jambo geni lakini kwa mwaka huu, mvua kubwa zimeshuhudiwa kutokana na mfumo wa hali ya hewa wa El-nino, huku Wataalamu wakisema mabadiliko ya tabianchi pia yamechochea hali hiyo ambayo imeleta madhara maeneo mengi.
Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, inaeleza kuwa Mvua kubwa na mafuriko vinavyoshuhudiwa tangu mwezi Machi, 2024 vimesababisha uharibifu mkubwa hapa Nchini lakini pia kwa majirani zetu Tanzania, Burundi, Somalia, Rwanda, Kenya na maeneo mengine ya Afrika.
Hata hivyo wapo wanaoelewa uhalisia na ambao wanahusisha moja kwa moja na aina fulani ya kutowajibika kwa Viongozi wa Mataifa, hali iliyopelekea Tume ya Haki za Binadamu nchini Kenya – KHRC, kuwashitaki Mawaziri watatu wa Serikali yao kwa uzembe na kushindwa kuwalinda waathirika wa mafuriko nchini humo.
Wakili wa KHRC, Kelly Malenya akihojiwa na Shirika la Habari la Ujerumani alisema waliwasilisha kesi yao Mahakamani Mei 17, 2024 kwa kuwashitaki Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, Waziri wa Mazingira, Soipan Tuya na Waziri wa Ardhi, Alice Wahome.
Malenya anasema, baadhi ya madhila na vifo vingeweza kuepukika ikiwa mamlaka ya Hali ya Hewa ya Kenya – KMD, ingetoa taarifa mapema, ili Waathiriwa wachukue hatua mapema na kudai kuwa pia Mwanasheria Mkuu, Justin Muturi, Shirika la Reli la Kenya na mashirika mengine kadhaa ya serikali yamehusishwa katika kesi hiyo.
Tume hiyo ya Haki za Binadamu inasema itapambania kuishinikiza Serikali kutoa msaada wa kibinadamu pamoja na fidia kwa wahanga wa mafuriko hayo yaliyosababisha vifo vya watu karibu 257 ma kupelekea uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo maporomoko ya udongo, uchafuzi wa vyanzo vya maji na mlipuko wa Kipindupindu.