Meneja wa Man Utd Jose Mourinho, amefunguliwa mashtaka na chama cha soka nchini England, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha wakati wa mchezo wa ligi wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Burnley uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bila kufungana.

Mourinho aliamrishwa kuondoka katika benchi la ufundi la Man Utd na mwamuzi Mark Clattenburg, baada ya kushindwa kuzitendea haki kanuni za ligi ya nchini England wakati wa mapumziko ya mchezo huo.

“Ni kinyume na sheria kwa yale aliyoyatamka katika eneo la kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia wakati wa mapumziko, alitoa lugha chafu na za kebehi dhidi ya waamuzi,” Ilieleza taarifa iliyotolewa na chama cha soka nchini England FA.

Mourinho amepewa muda wa kuwasilisha utetezi wake mpaka ijumaa jioni.

Katika hatua nyingine Mourinho hajawasilisha utetezi wa kupinga mashtaka ya kosa la kushurutisha mwamuzi Anthon Taylor kubadilishwa kabla ya kuchezesha mchezo wa ligi dhidi ya Liverpool, kwa kisingizio cha shinikizo lililokuwa limekithiri kwa mashabiki wa wa Man Utd na Liverpool kupitia mitandao ya kijamii.

Kufuatia hali hiyo meneja huyo kutoka nchini Ureno yupo katika hatari ya kufungiwa michezo miwili ama zaidi, sambamba na kutoruhusiwa kabisa kuingia uwanjani pale kikosi chake kitakapokua na jukumu la kusaka point tatu muhimu.

Live: Tazama Bunge la 11 leo Novemba 2, 2016
Nelson Cabrera Aiponza Bolivia, Yashushwa Hadi Mkiani