Mshambuliaji wa Man Utd, Marcus Rashford huenda akatajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England ambacho kitaingia kambini mwanzoni mwa juma lijalo.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate anatarajia kutangaza kikosi chake baadae hii leo, kwa ajili ya michezo ya kimataifa dhidi ya Ujerumani na Lithuania itakayochezwa juma lijalo.
Southgate anajipanga kuchukua maamuzi ya kumuita kikosini mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19, kufuatia taarifa za kuumia kwa mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane pamoja na Wayne Rooney wa Man utd.
Rashford aliripotiwa kuwa mgonjwa kabla ya mchezo wa robo fainali wa kombe la FA dhidi ya Chelsea, lakini kwa mshangao mkubwa alijumuishwa katika kikosi cha Man utd ambacho kilikubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Gareth Southgate alihudhuria Stamford Bridge kushuhudia mchezo huo, na alipomuona Rashford anacheza alionyesha kuridhishwa na uwezo wake.