Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, amefunguka kuwa, beki wa kati wa timu hiyo, Erasto Nyoni kwa sasa ndiye beki bora kwake kuliko wengine wanaocheza nafasi hiyo akiwemo Kelvin Yondani anayekipiga kwenye Klabu ya Yanga.
Mayanga ametoa kauli hiyo baada ya juzi Jumamosi kumpa nafasi Erasto anayekipiga kwenye Klabu ya Azam kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar na Taifa Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mbwana Samatta dakika ya pili na 87.
Akizungumzia umuhimu wa Erasto kwenye kikosi chake, Mayanga amesema: “Kiufundi namwamini sana Erasto na ndiyo maana nimemwita kwenye kikosi changu, lakini nafahamu nina idadi kubwa ya vijana wanaocheza kwenye safu ya ulinzi anayocheza yeye na sijawaita kutokana na sababu zangu binafsi.
“Sababu hasa iliyonifanya nimchukue Erasto, kwanza nilihitaji beki wa kati mzoefu, mrefu na mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, ukiangalia sifa hizo zote yeye anazo, hivyo kiufundi kwangu Erasto ni bora kwa sasa.
“Ninachowaomba Watanzania tuwaunge mkono wachezaji wetu na si kuwakatisha tamaa kwa sababu Tanzania ni ya wote na mwalimu anaangalia kwa wakati husika nani anafaa katika kuipigania timu.”
Chanzo: Championi