Serikali kupitia Chuo cha Usafirishaji (NIT) imedhamiria kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutekeleza azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Ili kufanikisha azma hiyo Serikali imepanga kutumia chuo hicho kuwa kitovu cha kuzalisha wataalamu watakaozalisha ajira na kuchangia kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Hayo yamesemwa mapema hii leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Angelina Madete wakati akizindua kozi za International Computer Driving Licence (ICDL) na Geographic Information System (GIS).
“Nimefarijika sana kusikia kwamba mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yajulikanayo kama International License (ICDL) yanayotolewa katika nchi zipatazo 100 kote duniani sasa yatapatikana katika Chuo chetu cha Usafirishaji (NIT) kwa gharama nafuu” amesema Madete.
Aidha, Madete amesema kuwa kwa sasa TEHAMA ikitumika ipasavyo itawanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii kupitia Sera Mpya ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2016.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo hicho amesema kuwa chuo hicho kimejipanga kujenga maabara 10 kwa ajili ya mafunzo (TEHAMA).
Naye mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Prof. Blasius Nyichomba amesema kuwa dhamira ya chuo hicho ni kuwa kitovu cha mafanikio ndio maana kimeweza kuwa na kozi zinazotambulika kimataifa.
Hata hivyo, amesema kuwa kozi zinazotolewa na chuo hicho zinalenga kutatua changamoto katika sekta ya Usafirishaji, Masoko,TEHAMA na nyingine kulingana na mahitaji ya wakati