Kocha mkuu wa mabingwa wa soka barani Afrika timu ya taifa ya Cameroon Hugo Broos, huenda akatangaza kujiuzulu nafasi hiyo kufuatia kuchoshwa na utendaji kazi wa viongozi wa shirikisho la soka nchini humo FECAFOOT.
Broos amesisitiza suala la mabadiliko katika soka la nchini Cameroon kwa muda mrefu, lakini hajaona mpango huo ukifanyiwa kazi ili kubadilisha mazingira ya maendeleo ya soka, ambayo yatawezesha baadhi ya mambo kusonga mbele.
Akizungumza na shirika la utangazaji la Uingereza BBC, Broos amesema amechoshwa na mwenenndo wa mabosi wake wa kushinda kusaka njia mbadala ambazo zitawezesha mabadiliko ya kiutendaji, hali ambayo anahisi inaweza kumkwamisha katika shughuli zake za kila siku.
Kocha huyo raia wa nchini Ubelgiji, amesema wakati kikosi chake kikipambana nchini Gabon mwanzoni mwa mwaka huu na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa AFCON, kila mmoja alionyesha kujituma kwa nafasi yake, lakini baada ya hapo mambo yamebadilika.
Broos ameibua malalamiko hayo kufuatia kikosi chake kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Guinea katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa jumanne nchini Ubelgiji, ambapo amedai matokeo hayo yalisababishwa na matatizo ya viongozi kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuihudumia timu ipasavyo.
“Wachezaji wangu hawapata chakula cha mchana kabla ya mchezo wetu na Guinea tuliocheza jumanne, na tulipofuatilia kwa maafisa wa hoteli tuliokua tumefikia pale Ubelgiji, tuliambiwa shirikisho la soka linadaiwa hivyo tumesitishiwa huduma ya chakula.”
“Mwaka mmoja uliopita, nilipoanza kazi hapa nilikuta matatizo lukuki, lakini nilijitahidi kufanya kazi yangu na hali ilibadilika siku hadi siku, lakini naona kwa sasa mambo yanaanza kujirudia tena,” Alisema Broos.
“Mfano wakati tunakwenda Afrika kusini kwa ajili ya kucheza mchezo wa kimataifa, wachezaji wangu pamoja na maafisa wa benchi la ufundi, tulilazimika kusubiri ndege kwa muda wa saa mbili, kwa sababu maafisa wa shirikisho walikua na dhamira ya kutaka kuongeza watu wengine katika msafara wetu, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za safari kwa timu kama Cameroon.
“Jambo lingine lililonikera katika utawala wangu ni daktari wa timu kushindwa kutimiziwa mahitaji yake, inafikia hatua viongozi wa shirikisho la soka nchini Cameroon wanashindwa kununua dawa kwa ajili ya wachezaji, jambo ambalo ni hatari.
“Tumewahi kusafiri bila ya kuwa na vifaa vya kufanyia mazoezi, na walipoulizwa viongozi walijibu, wanavifuatilia wakati walitambua timu inahitaji vifaa hivyo kwa wakati, ili mambo mengine yaendelee.”
“Kwa kweli siwezi kufanya kazi katika mazingira ya namna hii, nitafanya maamuzi wakati wowote.” Alisema Broos