Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), mkoa wa Dar es Salaam limeiomba Serikali kuwafikiria upya zaidi ya watu 9,000 waliofutwa kazi baada ya kubainika kuwa na vyeti feki.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TUCTA mkoa wa Dar es Salaam, George Faustine katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani maarufu kama Mei Mosi, yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta.
Faustine alisema kuwa TUCTA haiungi mkono vitendo vya kugushi vyeti, lakini mfumo pia uliokuwepo ndio uliotoa mianya hiyo.
“Wafanyakazi ambao wamebainika kuwa wamegushi vyeti, walifanya makosa. Lakini pia na mfumo wa kipindi hicho uliruhusu,” alisema Faustine.
“Kama mfumo huo ungekuwa halisi na sahihi, ungekuwa ‘genuine’ wasingeweza kuwasajili na hili nadhani lisingetufikia,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Mama Sitta aliwataka wafanyakazi kuendelea kuungana na kudai haki zao za msingi, huku akiwashauri kuwa sio lazima kwenye sherehe hizo kumualika waziri kuwa mgeni rasmi, bali wanaweza kuitumia siku hii kama sehemu ya kufanya mijadala kuhusu mambo yanayowakabili.
Maadhimisho hayo Kitaifa yalifanyika wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais John Magufuli ambaye aliambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai na viongozi wengine.