Kampuni ya ya michezo ya kubashiri matokeo ya SportPesa ya nchini Kenya imesaini mkataba mnono wa miaka mitano wa kuwa mdhamini mkuu wa klabu ya Everton inayoshiriki ligi kuu ya soka ya nchini England.
SportPesa inachukua nafasi ya kampuni ya Thai brewing Company Chang ya nchini Thailand ambayo imekuwa mdhamini mkuu wa Everton tangu mwaka 2004.
Mkurugenzi Mkuu wa Everton, Robert Elstone ameishukuru kampuni ya Sportpesa kwa kuipa klabu yake udhamini wa Pauni Milioni 75. Udhamini ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 140 ya uhai wa klabu hiyo yenye makao yake makuu jijini Liverpool.
Mbali ya kuidhamini Everton, Sportpesa pia imeripotiwa kuwa itaweka makao yake makuu kwenye jiji la Liverpool ambapo inatarajiwa kuwa itatoa ajira 100 katika kipindi cha miezi 18 ijayo.
Sportpesa ilizinduliwa nchini Kenya mwaka 2014 mpaka sasa imefanikiwa kuingia mikataba ya kuzidhamini klabu vitano za nje na ndani ya nchi ya Kenya.
Vilabu hivyo ni Gor Mahia, AFC Leopards (Kenya), Simba SC (Tanzania), Hull City na Everton (England).