Mshambuliaji hatari wa klabu ya Ruvu Shooting Abdulrahman Mussa amefungua milango kwa klabu za Simba, Young Africans na Azam FC kwa kuzitaka kufuata utaratibu kufanya mazungumzo ili kutimiza lengo la kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Abdulrahman ambaye kwa sasa ameshaifungia Ruvu Shooting mabao 13, amesema shughuli yake ni kucheza soka na linapokuja suala la kutakiwa na klabu yoyote kati ya Simba, Young Africans na Azam FC hana kipingamizi cha kuwaacha maafande wa jeshi la kujenga taifa.
Akizungumza na Dar24, mshambuliaji huyo amesema mkataba wake na klabu ya Ruvu Shooting utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, hivyo atakua huru kuondoka na kwenda mahala pengine kucheza soka lake.
“Mkataba wangu utafikia mwisho tutakapomaliza ligi hii, na niwaambie tu, viongozi wa klabu za Simba, Young Africans na Azam FC waje tuzungumze ili tupate muafaka ambao utanisaidia kujua ni wapi nitakapoangukia msimu ujao” Amesema Abdulrahman.
Hata hivyo amekiri kuwa, bado hajazungumza na uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting ili kuangalia uwezekano wa kusaini mkataba mpya, lakini bado akasisitiza yupo tayari kuondoka endapo klabu za Simba, Young Africans na Azam FC zitakua tayari kumsajili.
Abdulrahman Mussa hakutarajiwa kama angekua moto wa kuotea mbali dhidi ya safu za ulinzi za timu pinzani, lakini umahiri wake unaendelea kuwa gumzo katika vyombo vya habari kila kukicha.