Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) imejipanga kuwekeza katika sekta ya kilimo na mifugo visiwani Zanzibar kwa kuanza mchakato wa kutoa mikopo kwa wakulima na wakazi wa visiwani humo wanaojishughulisha na kilimo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Benki hiyo, Francis Assenga alipotembelea Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, visiwani humo amesema kuwa TADB ikiwa chombo cha Muungano ina wajibu wa kusaidia juhudi za Serikali katika kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania.
“Uanzishwaji wa TADB unatokana na Serikali kutambua umuhimu wa uwekezaji wenye tija kwenye maeneo yote ya sekta ya Kilimo na kuleta mapinduzi ya dhati ya Kilimo ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo na mitaji ya riba nafuu ikiwa ni pamoja na kuhamasisha mabenki na taasisi zingine za fedha nchini kutoa mikopo zaidi kwenye sekta ya Kilimo,” amesema Assenga.
Hata hivyo, Assenga amesema Zanzibar ina utajiri mkubwa kwenye uzalishaji wa viungo ‘spices’ ambayo ni mojawapo wa minyororo ya thamani ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao mbalimbali na Benki ya Kilimo.