Maafisa wa mifugo wote wa wilaya na mikoa wametakiwa kubadilika ili sekta hiyo iweze kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Juni 15, 2017 wakati akizungumza na maafisa mifugo kutoka wilaya zote na mikoa yote wanaohudhuria kikao alichokiitisha ili kujadili namna wanavyoweza kubadili uchungaji na kufanya uwe ufugaji.
“Katika ziara zangu za mikoani nimekuwa nikionesha kutoridhishwa kwangu na utendaji kazi wenu, na hasa jinsi tunavyoendesha ufugaji hapa nchini. Mmeacha kazi ya kuwaongoza wafugaji, wanafanya wanavyotaka. Tunahitaji kuona mabadiliko makubwa katika sekta hii,” amesema.
Majaliwa amesema takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika na ya 11 duniani kwa ufugaji, ikiwa na ng’ombe takriban milioni 24, nyuma ya Ethiopia yenye ng’ombe milioni 54 na Sudan yenye ng’ombe 41.
“Wakati sekta ya mifugo inatoa mchango usiozidi asilimia 10 kwenye Pato la Taifa, wenzetu Ethiopia sekta hiyo hiyo inachangia asilimia 14 kwenye pato lake na asilimia 16 ya fedha za kigeni. Nchi kama Botswana na Namibia, nazo zinafanya vizuri kwenye sekta ya mifugo, pamoja na kwamba wana mifugo michache, na eneo dogo la ardhi,” amesema.
Pia amewataka maafisa hao wabadili mitazamo yao na waache kufanya kazi kwa mazoea.
“Ni lazima mtafute ufumbuzi wa kudumu kuhusu utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji; na wafugaji na wahifadhi wa mapori tengefu au mapori ya akiba.”
Maafisa hao wametakiwa kujipanga kuongeza uzalishaji wa mitamba na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuendelea kuzalisha mitamba ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa.