Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewaonya Mawaziri ambao hawakuhudhuria katika ziara yake maalum ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika mkoa wa Mjini Magharibi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani, Dkt. Shein alionesha kuchukizwa na kitendo hicho kilichofanywa na mawaziri na kutoa onyo kali.
“Baadhi ya mawaziri wangu hawapo, wapo walioniaga wawili, wengine hawajaniaga. Nataka niwaone mawaziri wangu katika ziara hii. Nilisema juzi kule Tunguu na narudia tena… hii siyo ziara ya mchezo, ni ziara ya kazi. Wanachokitafuta watakipata,” alisema Dkt. Shein.
Baada ya hotuba yake, Dkt. Shein aliendelea na ziara yake ambapo alikagua shughuli za ujenzi wa kiwanja cha michezo uwanja wa Mao, Kikwajuni. Dkt. Shein pia aliendelea na ziara yake katika eneo Kilimani, Kizingo ambapo alikagua mradi wa kuzuia kasi ya Mawimbi ya habari.
- Ummy Mwalimu aagiza kuboreshwa kwa huduma za afya
- Naibu waziri ajiuzulu kwa kashfa ya kumpiga mwanamke
Maeneo mengine aliyatembelea leo ni pamoja na eneo la Maruhubi ambapo aliweka jiwe la msingi la jengo la Chuo cha Utalii na hatimaye kuzindua tawi la CCM katika eneo la Matarumbeta.
Dkt. Shein anaendelea na ziara hiyo ya kikazi katika mkoa wa Mjini Magharibi itakayokamilika Agosti 21 mwaka huu.