Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara klabu ya Yanga, imeteua kamati ya mabadiliko yenye watu sita akiwemo mkuu wa mkoa wa zamani wa Dar es salaam Mh. Meck Sadick.
Yanga SC imefuata nyayo za mahasimu wao, klabu ya Simba kwa kuunda kamati hiyo ya mabadiliko ambayo itasimamia mchakato wa kuelekea kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu.
Kamati hiyo inayoundwa na Mwenyekiti ambaye ni mwanasheria Alex Mgongolwa imetangazwa leo na Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo Clement Sanga kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Wajumbe wa kamati hiyo ni Prof Mgongo Fimbo ambaye ni mtaalam wa Katiba na sheria za ardhi, Meck Sadick ambaye ni mkuu wa mkoa wa zamani wa Dar es salaam, Mohamed Nyenge ambaye ni mchumi na Mwenyekiti wa kamati ya uchumi na fedha wa Yanga.
Wengine ni George Fumbuka akiwa mshauri wa masuala ya uwekezaji na Felix Mlaki ambaye ni mchumi na mtaalam wa masuala ya fedha. Yanga pia jana iliteua kamati ya mashindano yenye watu 28